Mfanyakazi wa ndani, Yusta Lucas (20)
amekumbana na masahibu yanayofanana na yale ya mtoto Nasra Mvungi (4) aliyekuwa
amefungiwa kwenye boksi kwa miaka karibu minne huko Morogoro. Huyu amelazwa
katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam akiuguza majeraha yanayotokana
na kuteswa na kufungiwa ndani kwa miaka mitatu.
Binti huyo, mwenyeji wa Mkoa wa Tabora, katika
Kijiji cha Kampala amedai kuwa amekuwa akiteswa na kufungiwa ndani ya nyumba na
tajiri yake, Amina Maige wa Mwananyamala, Kwa Manjunju katika kipindi chote
hicho.
Amina anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa tuhuma hizo na amefunguliwa jalada namba OB/RB/9967/2014.
Amina anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa tuhuma hizo na amefunguliwa jalada namba OB/RB/9967/2014.
Akisimulia masahibu yaliyompata akiwa katika
Wodi Namba Tatu ya hospitali hiyo, Yusta alisema: “Nililetwa Dar es Salaam
mwaka 2010 kufanya kazi za nyumbani baada ya bosi wangu (Amina) ambaye ni
binamu yangu kuzungumza na mama yangu na kuniomba nije kumsaidia kazi
ndogondogo.”
Alisema aliishi vizuri na mwajiri wake huyo,
lakini mwaka 2012 ndipo mambo yalipoanza kubadilika akidai kuwa Amina alianza
kumwadhibu kwa kumng’ata na kumchoma kwa pasi kila alipomtuhumu kutokufanya
kazi zake vizuri.
“Alikuwa akinichapa na kuning’ata sehemu
mbalimbali wakati mwingine usoni, pia kunichoma kwa pasi yenye moto kila
aliponituhumu kutokufagia au kupiga deki vizuri.”
Hakuwahi kupelekwa hospitali
Alisema licha ya kupata vidonda kutokana na
adhabu hizo, mwajiri wake huyo hakuwahi kumpeleka hospitali na pale alipoona
hali ni mbaya alimnunulia dawa... “Tunaishi wawili tu baada ya kuondoka
mumewe na mtoto wake kumpeleka shule ya bweni... niliugulia hadi nikapona bila
mtu mwingine kufahamu.”
“Akienda kazini anafunga geti na kunikataza
kufungua hata kama mtu atagonga… sokoni nilikuwa naenda siku ambazo yeye yupo
tu na huwa akiniamrisha niende haraka na kurudi pasipo kuzungumza na mtu
yeyote.”
Alisema mwajiri wake huyo alikuwa akituma pesa
za mshahara wake kwa mama yake akisema ndiye anayepaswa kulipwa, jambo ambalo
anadhani limemfanya mama yake kuhisi mwanaye yuko katika mikono salama... “Kila
alipotuma alipiga simu na kunipa niongee na mama kuhakikisha kama zimefika huku
akinisimamia na baada ya hapo anachukua simu.”
Ataka kurudi kwao
Binti huyo ambaye sehemu kubwa ya mwili wake
ina alama za kung’atwa meno na majeraha ya kuchomwa na pasi, alisema: “Ninaomba
mtu yeyote mwenye hela, nataka nikitoka hapa hospitali nirudi Tabora kwa mama.
Nina shaka na maisha yangu hapa kwa huyu mama… sitaki tena kubaki Dar es Salaam
kutokana na mateso ninayoyapata."
Polisi wasema
Mkaguzi Msaidizi wa Dawati la Jinsia Polisi
Mkoa wa Kinondoni, Prisca Komba alisema taarifa za binti huyo ziliwafikia baada
ya majirani kupeleka taarifa hizo katika Kikundi cha Kipange kilichopo Kwa
Manjunju ambacho nacho kilitoa taarifa polisi na ndipo mtego wa kumnasa
mwanamke huyo ukawekwa.
Majirani walichukua hatua hiyo kutokana na
kusikia kelele za kilio mara kwa mara zikitokea ndani ya nyumba ya mtuhumiwa. “Tumekagua
makovu na majeraha mbalimbali yaliyo katika mwili wake na kupata jumla kuwa
yako 91,” alisema Komba na kuongeza:
“Toka jana amekuwa akinitaka nisiondoke mbali
naye amekuwa na hofu, lakini sasa afadhali kidogo baada ya kumpatia ushauri na
kumhakikishia kwamba hapa yuko salama.”
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Thobias
Edoyeka alisema suala hilo linashughulikiwa na polisi pamoja na ustawi wa
jamii, kauli iliyoungwa mkono na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mwananyamala, Rose
Temu ambaye alisema wanafuatilia kwa karibu matibabu yake pamoja na usalama
wake. “Hali yake ikishaimarika na kujiridhisha kuwa anaendelea vizuri,
tutakuwa na jukumu la kumuunganisha na familia yake,” alisema.
Ofisa Muuguzi Msaidizi Wodi Namba Tatu ambayo
ni ya kinamama, Rose Mussa alisema Yusta anaendelea vizuri.
“Anaendelea vizuri kwa kweli, jana (juzi)
hakuwa hivi alikuwa mwoga hawezi kujieleza tofauti na leo (jana)… bado
anaendelea na vipimo, tutakapoona anafaa kuruhusiwa tutafanya hivyo na
kumkabidhi kwa ustawi wa jamii.”
Credit: Mwananchi
Credit: Mwananchi
0 comments:
Chapisha Maoni