WAKATI jamii ya Watanzania ikipigwa butwaa na
ukatili wa kutisha aliofanyiwa mtoto wa miaka minne kwa kufungiwa ndani ya
boksi kwa miaka mitatu mjini Morogoro, ukatili mwingine wa kutisha dhidi ya
watoto umeripotiwa mkoani Kagera.
Katika mkoa huo, mganga wa kienyeji ametiwa
mbaroni, akituhumiwa kumuua kwa kumnyonga, kumkata mikono na kumzika katika
nyumba yake.
Mganga huyo, Mujingwa John (20) amekiri mbele
ya jeshi la polisi kuhusika na mauaji ya mtoto Fausta Geofrey (8), mwanafunzi
wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kitunga kata ya Muhutwe, wilayani
Muleba.
Anatuhumiwa kwamba, alimkamata kwa nguvu akienda
shule na wenzake, akamuua, kumkata mikono, nyama ya mgongo, masikio na sehemu
za siri kwa lengo la kuibanika na kutengeneza 'uchawi’ wake, kisha akachimba
shimo na kuzika mwili ndani ya nyumba.
Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa
Polisi mkoa wa Kagera, George Mayunga aliyesema mganga huyo alikamatwa na
polisi kwa kushirikiana na wananchi, ambapo alikutwa akibanika viungo
alivyovikata kutoka kwa mtoto huyo.
Aidha, akiwa polisi, mganga huyo alipewa fursa
ya kueleza kilichotokea mbele ya waandishi wa habari, ambapo alidai alifikia
uamuzi wa kumuua mtoto huyo, kutokana na hali ngumu ya umaskini inayomkabili.
Alisema baada ya kumkamata mtoto huyo,
alimkaba shingo na kumvuta hadi katika nyumba aliyokuwa akiishi, akamnyonga
hadi kufa na baada ya kufa, alimkata ngozi ya mgongoni, mikono akianzia na
mkono wa kushoto aliodai una bahati, sehemu za siri na masikio.
“Nilimkamata mtoto na kumuua, maana niliona
nikikamata mtu mzima atanizidi nguvu na kupiga kelele,” alidai.
Alidai kuwa, “Nilipomaliza kumuua
nilichimba shimo chini ya kitanda changu nikamzika na kutandaza nyasi juu yake
ili isigundulike kama eneo hilo kuna shimo".
Mganga huyo aliyejitambulisha kuwa ni Msukuma,
alidai viungo hivyo ambavyo hadi polisi wanafika, alikuwa bado akivikausha,
angevichanganya na dawa ambayo angewapatia wateja wake ili iwasaidie
kufanikisha mambo yao, ikiwamo kupata bahati na utajiri na alitarajia kuuza kwa
Sh 500 kwa kila ujazo wa kijiko kimoja cha dawa yake.
Alisema hiyo ni mara yake ya kwanza kufanya
tukio la aina hiyo na kwamba alihamia Muleba mkoani Kagera miaka miwili
iliyopita akitokea Nyanguge wilaya ya Magu mkoani Mwanza. Alisema alirithi
uganga huo kutoka kwa babu yake mzaa mama na kuwa alianza uganga akiwa na umri
wa miaka minane na hakuwahi kwenda shule.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bisole katika
Kata hiyo wilayani Muleba, Khamis Hassan, akizungumzia tukio hilo baada ya
mauaji hayo, alidai muuaji alimkata mtoto huyo mikono yake miwili kabla ya
kumzika.
Hassan alisema kuwa tukio hilo ni la Mei 21
mwaka huu asubuhi katika kijiji hicho, wakati mtoto huyo akiwa na wenzake
wakielekea shuleni, ambapo inadaiwa aliitwa na kukamatwa na mganga huyo,
aliyetambulika kwa jina la Mujingwa John (20).
Alisema kuwa baada ya taarifa za mtoto huyo
kutoonekana kuzagaa, wanakijiji walikusanyana na kuanza msako, ambapo
walikamata kundi la watu waliokuwa wakiwahofia kuhusika, hasa vijana.
Alisema baada ya kuwakamata watu hao,
waliwaweka sehemu moja na kuwaita wanafunzi waliokuwa na marehemu, ambapo
walimtambua mganga huyo kuwa ndiye aliyemwita na kumkamata mtoto huyo.
Mtendaji huyo alidai baada ya mganga huyo
kutambuliwa, wananchi na polisi waliofika eneo hilo, walikwenda naye hadi
katika nyumba anayoishi na kumtaka awaonyeshe alipo mtoto huyo. Alidai baada ya
kumbana, aliwaonesha sehemu alikomzika, ambapo walichukua jembe na kuanza
kufukua mwili wa mtoto huyo, uliokuwa umezikwa ndani ya nyumba aliyoishi mganga
huyo.
Alidai baada ya mganga huyo kumuua mtoto huyo,
alimkata mikono yake miwili na kisha kuchimba shimo ndani ya nyumba, ambapo
baada ya kumzika alifukia shimo akatandaza nyasi juu yake na kisha kuweka
kitanda chenye godoro alilokuwa akilala.
Alisema kuwa alipohojiwa ili kujua nani
kamtuma kutekeleza unyama huo, mganga huyo alidai ilitokana na yeye kuoteshwa
na mizimu yake, iliyomtaka kumuua mtoto ili amkate viungo vyake kwa ajili ya
kuchanganya na dawa.
0 comments:
Chapisha Maoni