MSAKO
wa Fisi waliovamia makazi ya Vitongoji vitatu vya Kijiji cha Hungumalwa Kata ya
Hungumarwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza, umezua maajabu.
Maajabu hayo
yamehusishwa na imani za kishirikina, baada ya fisi wawili kati ya 12
waliouawa, kukutwa wamevalishwa shanga na Rozali, kiunoni.
Msako huo wasiku tatu
ulioanza juzi (Jumapili) unahusisha mamia ya wananchi wa Kijiji hicho na
vitongoji vyake vya Mwanzabalemi, Mwanega na Mwang’ombe, wanaotumia siraha za
jadi na mbwa wapatao 50.
Habari za ndani
kutoka Kijijini humo zimesema kwamba, kabla ya wananchi hao kuingia ‘vitani’
kusaka wanyama hao ambao baadhi wanadaiwa kumilikiwa na watu wachache
wanaojihusisha na vitendo vya ushirikina, wazee wa Kijiji na Vitongoji hivyo,
walifanya mazindiko (kinga) ya kujikinga na nguvu za washirikina ambazo zinge
kwamisha zoezi hilo.
Kwa mujibu wa baadhi
ya wazee wa kijiji hicho ambao hawakutaka majina yao yaandikwe, walisema kuwa
makamanda wa jadi wanaoongoza msakao huo pamoja na mbwa wao, wana kinga za
kupambana na imani za kishirikina vinginevyo wasingeweza kuua fisi wenye shanga
na Rozali wanaotumiwa kishirikina.
Diwani wa Kata ya
Hungumalwa Shija Malando akizungumza na waandishi katika Kijiji hicho jana,
alisema wananchi walifikia maamzi ya kufanya msako huo wa siku tatu, baada ya
kundi kubwa la Fisi hao wanaokadiliwa kuwa zaidi ya 80, kuwa tishio kwa watoto
na mifugo.
Alisema kuwa, kwa muda
wa miaka miwili iliyopita hadi sasa, licha ya wanyama hao kuharibu hekali moja
ya matunda aina ya Tikiti Maji yaliyokuwa yamelimwa na mwanchi mmoja, wameua
ng’ombe 109, Mbuzi 135, kondoo 127 na Nguruwe 15 katika Vitongoji hivyo.
“Njooni muone maajabu
haya.” Alisema Malando na kufafanua “Jana (juzi Jumapili) wananchi
walifanikiwa kuua fisi kumi wawili kati yao wakiwa na maajabu. Mmoja aliukuwa
na Rozali kiunoni na mwingine akiwa na shanga kiunoni huku uume wake ukiwa
umetahiriwa kama binaadam.”
Alisema fisi
waliokutwa na vitu hivyo kiunoni, kwa imani za kabila la Kisukuma, wanadaiwa
kumilikiwa na baadhi ya watu wenye imani za kishirikina na kwamba, waliuawa
majira ya saa 8 hadi saa 10 mchana kwenye eneo la mlima wa Mwanzabalemi.
Alifafanua kuwa, fisi
kumi waliuawa (jumapili) siku ya kwanza ya msako huo na wengine wawili waliuawa
jana asubuhi na kwamba maeneo ya milima ya Mwanangi katika Kijiji cha Buyobo na
Kitongoji cha Mwanzabalemi yanasadikiwa kuwa na fisi wengi zaidi.
“Pamoja na kushambulia
mifugo yetu, ilifika mahali wananchi walikuwa hawawezi kutembea kwa uhuru
nyakati za usiku na baadhi ya watoto wanaosoma mbali kukatisha masomo kwa
kuhofia kuliwa na fisi hao.” Alieleza Mwenyekiti wa Kijiji cha
Hungumalwa, Clement Kaswahili.
Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Mwang’ombe Joseph Kisena alisema hadi kufikia leo (siku ya tatu
ya msako huo) watakuwa wameua fisi wengi zaidi kutokana na ushirikiano mzuri wa
Vitongoji hivyo vinavyotumia mbwa 50 na silaha mbalimbali za jadi ikiwemo
mikuki, mapanga na marungu.
0 comments:
Chapisha Maoni