Wakati homa ya dengue ikizidi kusambaa nchini, tayari watu 60 wamebainika kuwa na dalili za ugonjwa huo mkoani Lindi, lakini jijini Dar es Salaam ameibuka kiongozi wa dini anayejiita nabii na kwamba anatibu ugonjwa huo kwa kutumia juisi.
Taarifa za kuwepo kwa nabii huyo anayejulikana kwa
jina la Yaspi Bendera, kumefanya baadhi ya wagonjwa kuanza kumiminika
katika kanisa lake la Ufunuo kwa Watu Wote lililopo eneo la Yombo
Buza-Kipera, Wilaya ya Temeke, wengine wakidaiwa kutoka hospitalini,
kwenda kupata ‘uponyaji’.
Lakini serikali imeonya dhidi ya vitendo vya
baadhi ya watu kuwaondoa wagonjwa hospitalini na kuwapeleka kwenye
maombi, ikisema mtu yeyote anayesababisha wagonjwa kuondolewa
hospitalini kwa ajili ya kwenda kufanyiwa maombi atachukuliwa kuwa ni
adui namba moja katika jitihada za kupambana na ugonjwa huo na
kusisitiza kuwa wagonjwa ni lazima kwanza watimize dozi wanazopewa na
wataalamu hospitalini ndipo waendelee na imani zao.
Wakati wataalamu wakisema kuwa ugonjwa huo
unatokana na mbu aina ya aedes egypti, Nabii Yaspi anadai kuwa homa ya
dengue ni pigo lililoletwa na Mungu kwa watu wasiotaka kumtii.
Nabii huyo alidai kuwa alionyeshwa na Mungu miezi
miwili iliyopita kuwa homa ya ugonjwa huo ingeibuka nchini na kwamba
itawaathiri zaidi watu wazima kuliko watoto.
Alidai kuwa moyoni ana siri nzito ambayo
atamwambia mkuu wa nchi peke yake na iwapo atakosa fursa ya kufanya
hivyo, hatamwambia mtu mwingine.
“Nina siri ambayo nataka kumwambia Rais Jakaya
Kikwete na tayari nimeshaomba kukutana naye. Kama akikataa sitamwambia
mtu mwingine yeyote,” alisema.
Nabii Yasp alitoa madai hayo huku ugonjwa huo
ukiwa ushaua watu sita na wengine 600 kuugua katika mikoa ya Dar es
Salaam, Pwani, Arusha, Shinyanga, Zanzibar na Lindi.
Inadaiwa kuwa mpaka sasa, nabii huyo ameshaponya watu sita kwa kutumia kinywaji cha juisi na maombi.
“Kuna mgonjwa wa dengue alikuja kanisani Jumapili
kuombewa akitoka wodini Muhimbili, baada ya maombezi alipona kabisa na
sasa ni mzima,” alisema.
Inadaiwa kuwa mgonjwa huyo aliambiwa na nabii
anyanyuke akashindwa, lakini baada ya kunyweshwa juisi hiyo na kuombewa
aliulizwa kitu gani hawezi kufanya na ambacho angependa kufanya wakati
huo, ndipo mgonjwa alijibu kuwa alitaka kutembea, nabii alimwambia
“simama utembee”.
Katika hali isiyo kuwa ya kawaida, Emmanuel badala
ya kutembea alianza kukimbia kwa furaha akizunguka kanisani.
Baada ya tukio hilo, mgonjwa huyo aliambiwa arudi hospitali akawajulishe madaktari kuwa amepona.
Baada ya tukio hilo, mgonjwa huyo aliambiwa arudi hospitali akawajulishe madaktari kuwa amepona.
Mgonjwa alirudi Hospitali ya Muhimbili kutolewa mpira kama
alivyokuwa ameshauriwa na nabii. Siku tano baadaye alikwenda kanisani
kumshukuru Mungu, huku akisimulia namna alivyowashawishi wagonjwa
wengine wa dengue kwenda kunywa juisi ya muujiza.
Kauli ya serikali ya mkoa
Lakini, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky
Sadiki amekemea kitendo hicho akisema mtu yeyote anayesababisha wagonjwa
watolewe wodini kwa ajili ya kwenda kuombewa, atachukuliwa kuwa adui
namba moja dhidi ya jitihada za serikali za kutokomeza ugonjwa wa homa
ya dengue.
Sadiki alisema mgonjwa anayetaka kwenda kuombewa
aende baada ya kumaliza dozi aliyoandikiwa na siyo kuondoka hospitalini
na kuacha dawa.
“Sitaki kuiingilia imani, lakini kumtoa mgonjwa
hospitali akaombewe hilo silikubali,” alisema mkuu huyo wa mkoa na
kuongeza kuwa baadhi ya watu wameanza kupotosha wananchi kuwa majani ya
mipapai yanatibu ugonjwa huo.
Mganga Mkuu Hospitali ya Temeke
Mganga mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dk Silvia Mamkwe
alisema ni vyema watu wakaheshimu imani zao, lakini siyo sahihi mgonjwa
wa homa ya dengue kuacha dawa kwa sababu ya maombi.
Alisema sheria za manispaa zipo wazi kabisa kuhusu
taratibu zinazotakiwa kufuatwa kwa mtu anayetaka kumtoa mgonjwa wodini,
kwa hiyo ni kosa mgonjwa kuondoka wodini kwenda kuombewa.
0 comments:
Chapisha Maoni