.

Jumamosi, 31 Mei 2014

INASIKITISHA SANA...MTOTO AFA MAJI AKIENDA KANISANI..SOMA ZAIDI HAPA...!



Mwili wa Prince lsaack ukiwa unaelea majini.MTOTO Prince lsaack (10) mwanafunzi wa darasa la 5, mkazi wa Kata ya Kihonda, Maghorofani mkoani hapa, amefariki dunia wakati akiogelea mtoni na wenzake.

Prince alifikwa na mauti Jumapili iliyopita saa 7 mchana wakati akienda kanisani lakini kabla ya kufika huko waliamua kuogelea katika Mto Ngerengere bila kujua hatari iliyokuwa mbele yake.
Akizungumza na Ijumaa kuhusiana na kifo hicho, mama mzazi wa marehemu, Sarah Mwanjaa alisema amehuzunishwa mno na tukio hilo.
Mama huyo aliongeza kuwa, amepata pigo kubwa sana kuondokewa na Prince ambaye yeye na mwenzake ndiyo walikuwa faraja yake kufuatia kufiwa na mumewe. Akizungumzia tukio hilo alisema kwamba siku ya tukio alimwambia marehemu ikifika saa 8 mchana ale kisha aende kwenye ibada ya watoto katika kanisa wanalosali la Tanzania Assembulies of God lililopo Mwembesongo.

“Kwa kuwa ibada ya wakubwa inafanyika saa 4 asubuhi nilimuaga, nikaelekea kanisani na kusisitiza ikifika saa nane awahi kanisani, nikaondoka bila kujua kama nilikuwa namuaga mwanangu,” alisema mama huyo.



Polisi wakiwasili eneo la tukio. Aliongeza kuwa, ilipofika saa 8 mchana hakumuona mwanaye kanisani akapata wasiwasi na kuamua kurudi nyumbani ambako alimkuta rafiki wa marehemu aitwaye Steve akiwa ameshika nguo za mwanaye akamwambia walikuwa wanaogelea lakini mwenzake alizama mtoni.

“Baada ya kupewa taarifa hiyo nilianza kulia ndipo walitokea majirani zangu nikawaambia kilichotokea, wakaenda kutoa taarifa kwa afisa mtendaji, Godfrey Maumba wakaanza kumtafuta bila mafanikio kwa muda wa siku tatu,” alisema mama huyo.

Aliongeza kuwa baada ya kumtafuta usiku na mchana bila mafanikio, siku ya nne alipatikana akiwa amekufa huku baadhi ya sehemu za mwili wake zikiwa zimenyofolewa na mamba.
Akizungumza na Ijumaa kuhusiana na tukio hilo, afisa mtendaji wa kata hiyo, Maumba alikiri kutokea tukio hilo na kusema wamepata pigo kubwa sana kumpoteza mtoto huyo mdogo.


Mwili ukitolewa majini. Naye Diwana wa Kata hiyo, Lydia Mbihaji akizungumza na paparazi wetu kuhusiana na tukio hilo alisema amesikitika sana na akatoa rai kwa wazazi kuwa makini na watoto wao. Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard Paulo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Prince na gazeti hili linaipa pole familia yake na kumuomba Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu.

0 comments:

Chapisha Maoni