.

Jumatano, 1 Oktoba 2014

Ajali ya gari Mbeya yaua watu watano wa ukoo mmoja






“Baada ya ajali ile baba, mama na watoto wawili walifariki dunia papo hapo, lakini mkuu wa chuo ambaye pia ni ndugu wa marehemu hao na mtoto wake wa darasa la pili walijeruhiwa.




Mbeya. Watu watano wa ukoo mmoja wamefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea Songwe, jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (Sia), Wilaya ya Mbeya Vijijini baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana na lori usiku.

Katika ajali hiyo iliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita, watu wanne walifariki dunia papohapo, huku Mkuu wa Chuo cha Ualimu cha St. Aggrey, Tawi la Mbeya, Sterwat Danda akifariki dunia wakati akipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili, wakati wa kuaga mwili wa marehemu aliyekuwa mkuu wa chuo hicho jana, mmoja wa wakurugenzi wa Taasisi ya St. Aggrey, George Mwambusi alisema ajali hiyo ilihusisha baba, mama na watoto wake wawili wakati wakitokea wilayani Mbozi kuja Mbeya mjini.

“Baada ya ajali ile baba, mama na watoto wawili walifariki dunia papo hapo, lakini mkuu wa chuo ambaye pia ni ndugu wa marehemu hao na mtoto wake wa darasa la pili walijeruhiwa. Baadaye mwalimu huyo alifariki dunia wakati mtoto wake anayesoma darasa la pili bado anaendelea na matibabu,” alisema Mwambusi.

Hata hivyo, Mwambusi alishindwa kuwataja majina wanafamilia waliofariki dunia, lakini akasema walikuwa wageni wa mkuu wa chuo hicho na kwamba walikwenda Mbozi kusalimia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alithibitisha kutokea ajali hiyo na kwamba majina ya marehemu wote yalikuwapo ofisini kwake, lakini yeye alikuwa msibani.

Habari kutoka eneo la Chuo cha St Aggrey zilidai kuwa kabla ya tukio hilo, mkuu huyo wa chuo alipata ugeni wa ndugu zake, akiwamo aliyekuwa baba yake mdogo kutoka kijijini kwao, Ilembula Mkoa wa Njombe na walimtaka awasindikize Mbozi kumtembelea mtoto wao anayefanya kazi huko. - See more at: http://winternews1.blogspot.com/2014/10/ajali-ya-gari-mbeya-yaua-watu-watano-wa.html#sthash.oO3irhr4.dpuf

0 comments:

Chapisha Maoni