
NI mara yangu ya pili kumzungumzia Baby Madaha katika safu hii. Nilimsifu kwa kadiri ninavyomfahamu, kwamba ni muimbaji mzuri na anayefanya kazi yake vizuri kabisa, hasa hivi sasa anapokuwa balozi mzuri wa nchi, kwani anafanya shughuli zake na meneja kutoka Kenya.
Hapa nyumbani licha ya muziki, lakini anafanya pia filamu na huko kote amekuwa akifanya vizuri. Ingawa hajafikia kiwango cha kuweza kumlinganisha na msanii mkongwe kama Lady Jaydee, bado ni haki yake kusema kuwa ni miongoni mwa wasichana mastaa wanaofanya vizuri katika muziki.
Mastaa wana mambo mengi sana, hasa kutokana na kauli au matendo yao kufuatiliwa sana, tofauti na watu wa kawaida ambao hawana umaarufu wowote. Wiki mbili zilizopita, Baby kupitia moja ya magazeti pendwa ya Global, alisema Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao ulimalizika mapema wiki hii, umemfanya ashindwe kupata hela, kutokana na kumbi za starehe kuwa zimefungwa.
Alisema kufungwa kwa kumbi hizo, kunasababisha ashindwe kuingiza mshiko, hivyo ni bora kama ungeisha apate kujiingizia kipato.Sijui watu wengine walivyoichukulia kauli hiyo, lakini kwangu ilikuwa na upungufu mkubwa, ulionifanya nitafute walau muda niweze kuwasiliana naye kupitia hapa, kwa sababu kwangu, yalikuwa ni maneno mazito yasiyo na maadili ndani yake.
Ni kweli, kila mmoja ana imani yake na inapaswa kuheshimiwa, lakini unapokuja kwa jamii kama yetu ya Kitanzania, ni jambo lisilo na busara kutamka maneno kama hayo, hasa kutoka kwa mtu anayetazamiwa kuwa mfano mzuri kwa wanaomzunguka.
Mfungo wa Ramadhani ni moja ya nguzo kuu tano za dini ya Kiislamu, sasa mtu mmoja mwenye jina anaposimama na ‘kuulaani’ mwezi huo, ni kama anayetaka kukufuru. Kwa kuiangalia juujuu kauli hiyo, unaweza kukutana na mambo kadhaa ya kujiuliza.
Ina maana Baby Madaha anategemea muziki wa jukwaani tu kuweza kujiingizia kipato? Vipi, hana tabia ya kujiwekea akiba ili kuzikabili nyakati ngumu?Kama majibu ya maswali haya ni ndiyo, basi kuna tatizo dogo linalomkabili mdogo wangu huyu na hivyo ni lazima ajitahidi kulitafutia dawa. Lakini mbaya zaidi, ni kutochunga mdomo wake kuzungumza mambo ambayo anaelewa kabisa yanawagusa watu, tena wengine wakiwa na imani kali.
Watu flani wajinga ambao mara nyingi hupenda kutumia jina la dini tukufu ya Kiislam kufanya uhalifu, wangeweza kuichukulia kauli hii kama kashfa kwa Uislam na kuweza hata kumsababishia matatizo yeye binafsi.
Lakini pia msanii mkubwa na mwenye mkataba wa kimataifa, hawezi kulalamikia shoo za jukwaani kama ndiyo chanzo chake kikubwa cha mapato. Nilitegemea kusikia akaunti yake ikiwa nono, hasa kutokana na tambo zake za mara kwa mara kuwa anapata malipo mazuri katika mkataba wake.
Kauli yake inaonyesha hana chanzo mbadala. Watu wanaopata fedha kupitia vipaji vyao, huwekeza pia katika miradi mingine kwa sababu vipaji ni kama mitaji. Msanii wa kuimba au kuigiza haiwezi kuifanya kazi hiyo miaka yote ya maisha yake.
Itafikia kipindi, kwa sababu zozote zile, mtu atashindwa kupanda jukwaani, utafanyaje?
Kama kwa mwezi mmoja tu msanii mwenye mkataba mnono analalamika njaa, vipi kama watu watahoji ubora wa mkataba wake anaodai kuwa nao? Wengine wanaweza kufikiri kuwa maneno yake ni ya uongo, yenye lengo la kujikweza wakati uhalisia wake hauko hivyo.
Nimshauri tu dada yangu kuangalia sana jinsi anavyoweza kucheza vizuri na kauli anazozitoa hadharani, hasa kwa heshima ya jina lake. Unapokuwa mtu maarufu, ni lazima ujue kila unyayo wako unapoinuka, watu wanauangalia tofauti na akina sisi ambao hata hatuwezi kuandikwa magazetini au kuonyeshwa kwenye runinga!
0 comments:
Chapisha Maoni