.

Ijumaa, 6 Juni 2014

SIKU ZA OMMY DIMPOZ KUFULIA ZIMEKARIBIA KAMA ATAENDELEA KUFANYA HAYA.

UNAPOTAKA kutaja majina ya vijana chipukizi, ambao sasa wanaogelea katika bahari ya ustaa , basi huwezi kuliweka mbali jina la Ommy Dimpoz , mkali wa vibao vikali vya Baadaye na Tupogo. Hizi ngoma mbili zimekimbiza sana na nadhani ndizo zinazompa shoo nyingi , ndani na nje ya nchi , ingawa pia hivi karibuni aliingiza mtaani kazi yake nyingine inayokwenda kwa jina la Ndagushima. Katika vitu huwa napenda , basi ni kujaribu kuwa mkweli kwa kadiri ninavyoweza. Mimi ni shabiki mkubwa wa nyimbo hizi mbili, ninazipenda sana kuzisikiliza ingawa sidhani kama zina ujumbe wa viwango hivyo .

Ni kazi za kiburudani zaidi , hasa unapokuwa umetoka kwenye kazi ngumu ya kufikirisha ubongo kama hizi zetu. Staili yake ya muziki imemfanya kuwa kipenzi kikubwa kwa mashabiki na ukichanganya na ubitozi wake , basi siyo jambo la ajabu kuona kwamba kwa muda mfupi tu tangu amepata jina kimuziki, amepata shoo nyingi nje ya nchi , kiasi cha kumfanya awe miongoni mwa mastaa wanaoingiza mkwanja wa kutosha , kama shoo za nje zinaweza kuwa kigezo cha kupata zaidi . Sijawahi kukaa na huyu bwana mdogo hata siku moja katika ile hali ya kubadilishana mawazo, hivyo sitatenda haki kama nitajaribu kumhukumu kwa mambo ambayo sina uhakika nayo , ingawa baadhi ya matendo mbele ya watu yanaweza kusaidia kutafsiri tabia ya mtu!



Jumapili iliyopita, Juni 1, 2014 dogo alikuwa miongoni mwa wasanii waliohudhuria shoo kubwa ya uzinduzi wa kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam uliofanyika katika Viwanja vya Mwembeyanga. Wasanii wengi walikuwepo na walifanya vizuri kwa kweli . Tatizo langu lilikuwa moja tu , kwa huyu chipukizi ambaye kama ataendelea kukaza buti kama hivi , basi haina shaka kwamba anaweza kuwa mojawapo ya alama za muziki wa kizazi kipya katika ulimwengu wa burudani . Wakati akipanda jukwaani , mashabiki kwa mamia , hawakuwa wamechangamka kama alivyotegemea na ili kuwaamsha, alivua kofia yake na kuwatupia .

Baada ya hapo akawatupia pia miwani. Hivi ni vitu vya kawaida kufanywa na mastaa wakubwa, inawafanya mashabiki kutambua jinsi gani mtu wao anavyowathamini . Na siyo wasanii wa muziki tu ambao hufanya hivi , wanasoka , wacheza tenisi, mabondia, madereva wa magari, wanariadha na wanamichezo wengine , huwarushia jezi , kofia na vitu vidogovidogo mashabiki wao . Ommy Dimpoz alifanya zaidi . Baada ya kutupa vitu hivyo na kukuta mashabiki wakiwa bado hawajapanda mzuka, alitoa shilingi elfu hamsini na kuwarushia.

Pata picha ya patashika iliyotokea kwa mashabiki. Unajua alichokisema ? “Sisi wasanii tunapata fedha nyingi kutoka kwenu nyinyi mashabiki wetu, kuonyesha kuwajali , naomba niwarudishie.” Hiyo tisa , kumi, Dimpoz alizama tena ‘ chimbo ’ na kuibuka na kiasi cha kama laki mbili hivi na kuwarushia tena watu waliojazana mbele yake ! Dah, sawa , wasanii wanapaswa kurudisha sehemu ya mapato yao kwa jamii, lakini sidhani kama ni kwa staili hii . Binafsi naona kama huu ni ushamba fulani hivi ! Mtu smati kichwani hawezi kutupa hela kwenye umati wa watu , tena wa uswahilini kama wa kule Temeke , unataka nini?

Naamini kabisa akitokea mtu hata kwenye kumbi ambazo tunajua zina watu wa afadhali , wenye uwezo wa kutoa kiingilio cha shilingi laki moja kama pale Mlimani City, bado akiibuka ‘ mtu wa mawe ’ na kurusha mahela itakuwa mshikemshike , sembuse Mwembeyanga? Zipo namna za kurudisha hela kwa jamii yako , siyo kwa wasanii tu , bali hata wafanyabiashara, kama wanavyofanya baadhi yao kama Dr . Reginald Mengi na Mzee Mustafa Sabodo.

Tafuta sehemu yenye shida ya maji , chimba kisima , angalia wenye shida ya huduma za afya, jenga zahanati au nenda katika vituo vya watoto yatima wape nguo , madaftari au hata kula nao chakula . Jamii yetu ina maskini wengi , kuwatupia hela kama vile huwasaidii , bali utawaumiza kwa sababu wataishia kugombana, kutoana ngeu na mwisho wa siku hakuna atakayeondoka na pesa kwa sababu zote zitachanika katika purukushani . Naamini kwa nilichokisema , Dimpoz atakuwa amenielewa. Source: Globe

0 comments:

Chapisha Maoni